INGIA HAPA KUSOMA HISTORIA YA HIP HOP ILIPOANZIA WAANZILISHI NA MENGINE MENGI
1.
MAANA YA HIP HOP
Mahali ilipozaliwa?
Julai 23 mwaka 2007, Jiji la New York, lilitangaza rasmi kuitambua 1520
sedgwick Ave iliyoko Bronx kuwa sehemu ambayo hip hop ilizaliwa. “1520
sedgwick Avenue ni sehemu ambayo Recreation Room, chumba alichokitumia
muasisi wa hip hop, Dj Cool Herc. Taarifa ilisema “ingawa kwa sasa
(wakati huo mwaka 2007) umefungwa kwa marekebisho tangu mwaka uliopita,
tunawataka wana hip hop na wawezeshaji wengine kutoa zabuni ya kupata
uendeshaji wa sehemu hii. Leo hii waratibu watafanya mkutano wa
waandishi wa habari katika eneo la kihistoria kutangaza kuwa Jimbo la
New York kupitia ofisi ya kuhifadhi makumbusho na utunzaji wa historia
wameyakubali maombi yaliyotumwa Julai 2 kuitambua rasmi sehemu hii”.
Dj Kool Herc
Ambaye ni mmoja kati ya waasisi wa Hip Hop anasema “sehemu nilipoanza
kupiga muziki ilikuwa ni 1520 Sedgwick Avenue, katika recreation room,
chumba kilichokuwepo katika jengo lilipokuwa pango langu, watu walikuja
kucheza muziki kutoka maeneo jirani”
Krs One
Anasema
“.mwaka 1973, nilikuwa Bronx, katika hii sehemu iliyoitwa 1520 sedgwick
Ave, hii ndiyo sehemu ambayo hip hop ilipozaliwa. Mtu anayeitwa Cool Dj
Herc alikuwa akifanya maenesho..”
Tarehe ya kuzaliwa
August 11, 1973, ndiyo tarehe ambayo hip hop ilizaliwa kwa mujibu wa
Cindy Campbell ambaye ni dada yake na Dj Kool Herc. Onesho la kwanza la
hip hop lilifanyika siku hiyo. Onesho hilo liliandaliwa na Dj Kool Herc
kwa lengo la kuchangisha pesa ili dada yake (Cindy Campbell) aweze
kurudi shule (back to school party). Herc alikodisha recreation room kwa
dola ishirini na tano za kimarekani na kiingilio ilikuwa ni thumni
(cent) 25 kwa wanawake na thumni 50 kwa wanaume. Herc alikuwa kwenye
mashine na msema chochote (mc) wa siku hiyo alikuwa ni dada yake
(cindy), tukio hili ndilo linalomfanya cindy Campbell kuwa mwanamke wa
kwanza katika hip hop (first lady of hip hop).
Charlie Ahearn
Ni mtu ambaye aliyeandaa filamu ya Hip Hop iitwayo “Wild Style” kuanzia
mwaka 1980 mpaka 1982 ilipotoka. Anasema “August 11, 1973 imeibadilisha
dunia, tunatakiwa kusherekea ubunifu na maajabu ya usiku huo”
Licha ya tarehe hiyo Universal Zulu Nation kupitia tovuti yao
wanaitambua tarehe 12 Nov 1973 kama tarehe rasmi ya kuzaliwa hip hop na
pia mwezi November kama mwezi rasmi wa hip hop. Wanasema “ kwa
kuzingatia tarehe tajwa hakuna kitakachokuwa na umuhimu kama
kusherehekea utamaduni wa hip hop na historia yake katika mwezi novemba,
hakika ndiyo kitu kilichotufanya Universal Zulu Nation tuwepo kwa zaidi
ya miaka ishirini na saba (kwa wakati huo)”
WATU NA VYANZO MBALIMBALI
VILIVYOWAHI
KUFAFANUA HIPHOP
Baadhi ya watu na vyanzo mbalimbali vya habari vimewahi kufafanua Hip
Hop kwa nyakati tofauti tofauti kulingana na mapokeo.
Wafuatao/vifuatavyo ni vyanzo na watu mbalimbali waliowahi kufafanua
maana ya hip hop:-
AFRICA BAMBATAA
“Hip hop ni
harakati za utamaduni mzima. Unapoongelea kughani (rap), kughani ni
sehemu ya utamaduni wa hip hop. Ughanaji (emceeing), umanju (deejaying),
uvaaji, lugha vyote hivi ni sehemu ya utamaduni. Wavunjaji (break
dance), namna unavyotenda, unavyokwenda, unavyotazama (mambo) ni sehemu
ya utamaduni na muziki wake hauna ubaguzi rangi. Muziki wa hip hop
umetokana na weusi, udhulungi, njano, nyekundu, nyeupe……. ni sehemu za
hip hop”.
DJ KOOL HERC
“Hip hop ni kemia (chemistry)
ambayo imetoka Jamaika.. nilizaliwa Jamaika na nilikuwa nasikiliza
muziki wa kiamerika nikiwa huko huko. Msanii niliyekuwa nikimpenda ni
James Brown. Ndiye aliyenivutia mimi, nilikuwa nikicheza vibao vingi vya
James Brown. Nilipokuja hapa (Bronx) nilijiweka katika mtindo wa
kiamerika ili kuendana na mazingira. Niliweza kukata midundo na kuicheza
kwa muda mrefu na watu wakaipenda, niliwapa ladha waliyoipenda……’’
DAVEY D
“Hip hop ni utamaduni ambamo ughanaji (rap) ndimo umeasisiwa. Mwanzoni
ulikuwa na nguzo nne ambazo ni sanaa ya machata (graffiti art),
mavunjanji (break dancing), umanju (dj) na emceeing (ughanaji). Hip hop
ni mtindo wa maisha ambao una lugha yake, mtindo wa kuvaa, muziki wake
na fikra zake hukua kila siku. Siku hizi machata pamoja mavunjaji
havitiliwi maanani sana ndio maana neno “rap” na “hip hop” yanatumika
kwa pamoja kumaanisha kitu kimoja lakini ikumbukwe kila nguzo zina
umuhimu na zinaendelea kuwepo katika utamaduni”
Anaendelea kusema
“tatizo ni kuelewa maana ya hip hop, mara nyingi huwa inatolewa na
wazungu (whites) wenye vyombo vya habari au wale ambao huwa wanapata
nafasi ya kuhojiwa katika vyombo hivyo. Huwa wanaelezea maana ya hip hop
kwa manufaa yao na sio kwa manufaa ya uma na wale waliouasisi utamaduni
huu wa hip hop”
COMMON
“Hip hop ni njia yetu ya kujieleza
(expression). Niliipenda mapema zaidi pindi tu ilipotambulishwa (hip
hop) kwangu. Nilisikia “the message” ya Melle Mel… nilipenda namna
alivyowasilisha na nilipenda pia alichokuwa akikisema
SAMIA X
Samia X ni mmoja kati ya waasisi na waanzilishi wa kundi la KWANZA UNITY amewahi kusema
“ Hip Hop ni sayansi ya upangaji vina katika midundo kuelezea maisha
yanavyoendelea katika jamii, Maisha….. ni msigishano na mpambano
unaoendelea kati ya miundo miwili tofauti kutafuta uwiano sahihi kama
giza na mwanga, starehe na shida,
protini na wanga, majani na miiba ”.
Maneno hayo aliyatoa wakati akifanya utangulizi katika santuri ya “vina
mwanzo, kati na mwisho” ya mwanamuziki Farid Kubanda maarufu kama Fid
Q.
WIKIPEDIA
Katika mtandao huu, Hip Hop imeelezewa
kama mfumo wa kuwasilisha mawazo kwa kutumia sanaa ya muziki ambao
utamaduni wake umeasisiwa kutoka katika jamii za wamarekani weusi na
walatino katika miaka ya 1970 jijini New York hususani katika South
Bronx. Kwa mujibu wa mtandao huu, Hip Hop imeorodheshewa misingi mitano
ambayo ni Ughanaji(mceeng), mavunjaji (break dancing), machata
(graffiti) ambayo imenukuliwa toka kwa Afrika Bambaataa. Msingi wa tano
unatajwa kuwa ni Mdundo kinywa (beat boxing).
WISEGEEK
Tovuti hii inaelezea Hip Hop ni harakati za utamaduni ambao mara nyingi
huwa katika mfumo wa muziki. Utamaduni huu ulianzia Bronx katika jiji
la New York katika miaka ya 1970. Utamaduni huu ulianza katika jumuiya
za wamarekani weusi ukapewa mchango mkubwa na jamii za walatino katika
ukuaji wake.
Utamaduni wa Hip Hop ulianza kama mtindo wa maisha
uliokuwa handakini kabla ya kuibuka na kuwa moja kati ya mikondo mikuu
ya maisha duniani. Mfumo huu umejipatia umaarufu mkubwa kwa kuwa umekua
ukifanywa kibiashara hususani katika taifa la marekani. Hip Hop
inaelezewa kama ni aina ya muziki ambayo inayohusisha vitu vingi katika
uwasilishwaji wake lakini mara nyingi huwahusisha zaidi manju na
mghanaji.
Katika tovuti hii imetaja nguzo za Hip Hop ni Djing,
Emceeing, break dancing na sanaa ya Graffiti. Inaelezewa pia wakati
mwingine Hip Hop Fashion, mdundo kinywa (beat boxing), Hip Hop Slang,
Street Knowledge na Street Enterpreneurship zimekua zikiongezwa kama
nguzo ya tano.
Kwa ujumla
Naweza kusema, “Hip Hop ni
utamaduni ambao huegemea katika kuwianisha kwa usahihi mambo kwa kutumia
zaidi kanuni za kisanaa kurahisisha milinganyo halisi inayoikumba jamii
husika kwa kutoa taarifa, maarifa na njia katika kusaidia harakati za
ukombozi wa tabaka fulani linalogandamizwa”.
Muasisi wa
utamaduni huu anafahamika kama Clive Campbell au kwa jina maarufu kama
Dj Kool Herc. Alikuwa ni manju(dj) mwenye asili ya Kijamaika aliyehamia
nchini marekani katika Bronx mwishoni mwa miaka ya 1960. Asili ya
utamaduni huu wa Hip Hop, unatoka kwa vijana weusi wa kimarekani pamoja
na walatino walioishi Bronx katika miaka ya 1970. Kwa wengi unatambulika
kuwa unatokana na wamarekani weusi kutokana na mchango mkubwa walioutoa
katika jitihada za kuikuza hip hop. Licha ya kuanzishwa na watu weusi
utamaduni huu wa Hip Hop unaweza kufanywa na mtu yeyote yule bila kujali
itikadi za kidini, kikabila, rangi, lugha au utaifa wa mtu.
Jina la Hip Hop lilikuja miaka michache baadaye utamaduni huu ulipokomaa
na kuwa mtindo rasmi wa maisha. Katika miaka ya sabini utamaduni huu
uliweza kupata kufafanuliwa nguzo zake nne za mwanzo kabla ya tano
kuongezeka. Kwa mara ya kwanza ziliorodheshwa na Afrika Bambaataa. Nguzo
hizo zilikuwa ni Uchenguaji/ughanaji (mceing), Umanju(deejaying),
mavunjanji (break dance) na machata (graffiti).
Maneno yaliyo
katika maana ya Hip Hop hapo juu ukitumia mawanda mapana utagundua yana
maana kubwa kama ambavyo yanavyoelezewa katika aya zinazofuata.
.........itaendelea....
No comments:
Post a Comment